BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Charles Boniface Mkwasa Jumanne ya Julai 26, anatarajia kutangaza kikosi kwa ajili ya kambi ya awali ya wiki moja ikiwa ni maandalizi ya kucheza na Nigeria katika mchezo wa kukamilisha ratiba ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Mkwasa  alisema lengo la kambi hiyo itakayoanza Agosti mosi ni kuwaweka sawa kisaikolojia wachezaji kabla ya kuita kambi nyingine rasmi wiki ya mwisho ya Agosti kujindaa na mchezo dhidi ya Super Eagles  unaotarajiwa kuchezwa Lagos Septemba 2.


“Kikosi changu kitakuwa na vijana wengi, mimi ni muumini mkubwa wa soka la vijana ambao baadhi niko nao na ambao nitawaita, lakini pia mara baada ya ligi kuanza, nitaangalia wengine kabla ya kuwa na program ya ratiba ijayo ya michuano mbalimbali ya kimataifa itakayotolewa na CAF na FIFA,” alisema Mkwasa.

Taifa Stars ilipangwa kundi G pamoja na timu nyingine kama Nigeria, Chad na Misri ambayo tayari imefuzu baada ya kukusanya pointi 10, Nigeria ina pointi mbili; Taifa Stars ina pointi moja wakati Chad ilijitoa katikati ya mashindano na kukatisha ndoto za Tanzania kucheza fainali hizo.

Post a Comment

 
Top