BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
MFANYABIASHARA Mohammed Dewji 'MO' amejitokeza hadharani na kukiri yupo tayari kufanya uwekezaji wa bilioni 20 kwa klabu ya Simba endapo wanachama wa klabu hiyo wataridhia.

Mo amekuwa akihusishwa na kutaka kufanya uwekezaji huo mkubwa ndani ya Simba huku baadhi ya wanachama wa klabu hiyo wakionekana kutokuwa tayari kutokana na sababu zao binafsi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake jijini Dar es Salaam MO alisema kinachomvutia kufanya uwekezaji huo mkubwa kwa Simba ni mapenzi aliyonayo kwa klabu hiyo huku akijaaliwa kipato kikubwa na Mungu.

"Simba naipenda toka moyoni, niliwahi kuidhamini miaka ya nyuma na tulifanya vizuri sana katika michuano ya kimataifa kila mwanasimba analijua," alisema MO.

Aidha Mo alisema bajeti ndogo ya Simba ndiyo inayoifanya klabu hiyo kushindwa kushindana katika solo la usajili na kutowalipa vizuri wachezaji kama ilivyo kwa Yanga na Azam.

Wakati huo huo MO alisema ndani ya miaka mitatu endapo atakubaliwa  kufanya uwekezaji atajenga kiwanja bora cha mpira, hosteli, Gym na kuajiri kocha mwenye vigezo.

Simba inatarajiwa kufanya mkutano mkuu wa wanachama utakaojadili juu ya uwendeshwaji wa klabu hiyo siku ya Jumapili katika Bwalo la maofisa wa Polisi Oysterbay.

Post a Comment

 
Top