BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda, Dar

MPIRA si uadui, ndio kauli iliyotawala katika shughuli ndogo iliyofanyika nyumbani kwa msemaji wa Simba, Haji Manara ambapo mashabiki wa Yanga wakiongozwa na msemaji wao Jerry Muro walikwenda kumkabidhi mchango wao.

Manara alitoa taarifa juma lililopita kuwa jicho lake moja limepoteza uwezo wa kuona  na kwamba analazimika kwenda kupatiwa matibabu nje ya nchi ambayo gharama zake zinakadiriwa kufikia dola 10,000 ambazo ni zaidi ya Sh 20 milioni.


Baada ya taarifa hizo mashabiki wa Yanga wakiongozwa na Muro waliamua kuchangishana na kufanikiwa kukusanya kiasi cha Sh 1,055,000 ambazo wamemkabidhi Manara usiku huu kama pole na mchango wao kwenye gharama hizo za matibabu.

Akizungumza na BOIPLUS nyumbani kwake Magomeni jijini Dar es Salaam, Manara alisema "Nawashukuru sana kwa mchango wenu, mnaweza kuona ni kiasi kidogo lakini mmefanya jambo ambalo ndilo linastahili kufanyika, mpira si uadui, zamani ndio ilikuwa hivi tatizo la Simba linatatuliwa na Yanga na tatizo la Yanga linatatuliwa na Simba."


Kwa upande wake Muro alimhakikishia Manara kuwa Yanga wapo pamoja nae na watamsindikiza hadi uwanja wa ndege huku wakimuombea arejee salama waendeleze mapambano .

Manara anatarajiwa kwenda nchini India siku chache zijazo kwa ajili kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu ya matatizo ya macho.

Post a Comment

 
Top