BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar

SIKU moja baada ya Kamati ya maadili ya shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) kumfungia mwaka mmoja kutojihusisha na masuala yoyote ya mpira, Mkuu wa kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga Jerry Muro leo ameibuka na kudai hatambui hukumu hiyo.

Kamati hiyo iliyoketi jana chini ya Mwenyekiti Wakili Wilson Ogunde ilimfungia Jerry mwaka mmoja na faini ya shilingi milioni tatu baada ya kukutwa na makosa matatu likiwemo kuhamasisha mashabiki wa Yanga kukaa upande wa watani wao Simba katika mchezo wa kombe la shirikisho dhidi ya TP Mazembe kitu ambacho kingeweza kuhatarisha amani.

Akizungumza na kituo kimoja cha Radio asubuhi hii Jerry alisema kamati hiyo haina mamlaka ya kumfungia kwakuwa haikumuajiri na wala yeye sio mwanachama wa TFF.

"Hawana mamlaka ya kunifungia kwavile mimi sio mwanachama wao na wala hawakuniajiri wao, mimi sio msemaji wa TFF ni msemaji wa Yanga," alisema Jerry.

Aidha Jerry alisema ataendelea kuwa msemaji wa Yanga mpaka muajiri wake atakapoamua au Sekretarieti ya klabu hiyo kuachana nae na sio mtu yoyote nje ya hapo.

"Mimi nitaendelea kuwa msemaji wa Yanga hadi viongozi wangu watakaposema hawanihitaji tena na wala sio TFF," alisema Jerry.

Wakati huo huo Jerry amewataka wapenzi na mashabiki wa Yanga kuwa watulivu kipindi hiki ambacho suala lake linashughulikiwa.

Post a Comment

 
Top