BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda

MWADUI wameamua, kama ulidhani ni Yanga, Simba na Azam pekee ndizo zinatisha huko sokoni basi umeingia 'chaka', klabu ya Mwadui FC leo imefanya balaa baada ya kuwashusha mgodini nyota takribani wanane wakiwemo wapya na wa zamani.

Taarifa ambazo BOIPLUS imezinasa kutoka chanzo chetu ndani ya wazee hao wa mgodini ni kwamba beki wa Kagera Sugar, Salum Kanoni tayari amesaini mkataba wa mwaka mmoja kujiunga na Mwadui sawa na Said Nassor 'Chollo' ambaye msimu uliopita alikuwa Stand United.


Kanoni alipoulizwa sababu iliyomfanya aachane na Kagera alisema "Nimekuwa ndani ya Kagera kwa kipindi kirefu sana, nadhani sasa nahitaji changamoto mpya ndio sababu nimeona nije Mwadui."

Beki Joram Mgeveke ambaye alikuwa klabuni hapo kwa mkopo akitokea Simba SC, amemaliza mkataba wake na wekundu hao na 'fasta' Mwadui wamemweka chini huku taarifa zikisema kuna uwezekano mkubwa akawa amesaini mkataba leo sambamba na kiungo Hassan Kabunda na beki Iddy Moby ambao wanaongezewa mikataba klabuni hapo.


Wakati huo huo BOIPLUS inajua kuwa kiungo wa Toto African, Abdallah Seseme yupo Shinyanga na atamalizana na Mwadui muda wowote kwavile mazungumzo yao yameshafikia pazuri. 

Mwadui pia iko mbioni kuvunja ukuta wa Coastal Union kwa kumalizana na walinzi Abdallah Mfuko na Adeyum Saleh huku pia David Luhende na Kevin Sabato wakionekana katika maeneo ya kujidai ya wachimba madini hao kuashiria kuna 'dili' ya kuongezewa mikataba.

Post a Comment

 
Top