BOIPLUS SPORTS BLOG

ACRA,Ghana
NDOTO za timu ya Yanga kufika katika hatua ya nusu fainali ya kombe la shirikisho barani Afrika zimefutika rasmi baada ya kukubali kichapo cha magoli 3-1 dhidi ya wenyeji Medeama FC.

Yanga ambao walitakiwa kuibuka na ushindi katika mchezo huo walifungwa goli la mapema dakika ya saba na beki Moses Amponsah kabla ya golikipa Deogratius Munishi kupangua penalti dakika moja mbele kutokana na Nahodha Nadir Haroub kumchezea rafu mshambuliaji Enock Agyei.

Dakika ya 22 mshambuliaji Abbas Mohammed aliwapatia wenyeji bao la pili kutokana na kukosekana kwa umakini wa mabeki wa Yanga kabla ya Simon Msuva kuwafungia wageni goli kwa mkwaju wa penalti kufuatia Obrey Chirwa kuangushwa katika eneo la hatari.

Abass tena alifunga goli la tatu baada ya mabeki wa Yanga kushindwa kuokoa mpira wa kona na kumkuta mfungaji akiwa hana mtu wa kumkaba huku mlinda mlango Dida akiwa hana la kufanya.

Yanga imebakiwa na michezo miwili dhidi ya Mo Bejaia mchezo utakaopigwa jijini Dar es Salaam kabla ya kusafiri kuelekea Lubumbashi kucheza na TP Mazembe.

Mpaka sasa Mazembe wanaongoza wakiwa na alama 7 wakifuatiwa na Bejaia wenye 5,Medeama 4 huku Yanga wakiburuza mkia wakiwa na alama moja pekee.

Kesho Mazembe watawakaribisha Bejaia katika mchezo wa kundi A huku wenyeji wakiwa na nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi.

Post a Comment

 
Top