BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar

LICHA ya kulazimishwa sare ya goli 1-1 na Medeama kocha wa timu ya Yanga Mholanzi Hans Van Pluijm anaona kuna uwezekano mkubwa wa kikosi chake kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali ya kombe la shirikisho barani Afrika.

Kimahesabu inaonekana mabingwa hao wa ligi kuu Tanzania bara hawana nafasi baada ya kijikusanyia alama moja huku wakiwa na michezo miwili ugenini na mmoja nyumbani dhidi ya Mo Bejaia ambao waliwafunga katika mchezo wa awali.

Pluijm ameongea na vyombo vya habari baada ya kumalizika kwa mtanange huo huku akionekana kujiamini na kusema vijana wake walicheza vizuri lakini tatizo la kutokutumia nafasi wanazopata linaendelea kuwaandama.

"Ukiniuliza kuwa tunaweza kufuzu katika hatua ya nusu fainali jibu lake ni ndiyo kwakua katika mpira kila kitu kinawezekana,tumebakiwa na mechi tatu na tukishinda zote tutakuwa na alama kumi," alisema Hans.

Kwa upande wake kocha wa Medeama, Pride Yaw Owusu alisema wapinzani wao walikuwa bora zaidi ila waliwabana kwa kutumia faida ya kucheza mechi ya ugenini na kufanikiwa kupata alama moja.

"Tulicheza kwa tahadhari kubwa kwakuwa tupo ugenini, Yanga walikuwa wazuri lakini tunarudi nyumbani kujipanga na michezo mingine iliyo mbele yetu" alisema Owusu.

Timu zote mbili zina nafasi ndogo ya kupita katika kundi lao linaloongozwa na TP Mazembe ambao watashuka dimbani kesho kucheza na Mo Bejaia wenye alama nne wakishika nafasi ya pili.

Post a Comment

 
Top