BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu, Dar
UONGOZI wa Maafande wa Ruvu shooting umeachana na kocha wake Mkenya Tom Olaba baada ya kudumu nae kwa miaka miwili katika viunga vya Mabatini Kibaha mkoani Pwani.

Hatua hiyo inakuja muda mchache baada ya Mkenya huyo kuipandisha daraja timu hiyo ambayo ilishuka msimu wa 2015/16 na kushiriki daraja la kwanza kabla ya kurejea tena msimu huu.

Uongozi wa klabu hiyo kupitia kwa Mwenyekiti wake Kanali Charles Mbuge umesema Olaba ni miongoni mwa makocha bora waliowahi kuifundisha timu hiyo na wataendelea kuthamini mchango wa Mkenya huyo ndani ya Maafande wa Ruvu shooting.

Ofisa Habari wa klabu hiyo Masau Bwire alisema timu hiyo kwa sasa ipo chini ya kocha Selemani Msungwe ambaye amerithi mikoba ya Mkenya huyo na tayari amekwishaanza maandalizi kuelekea msimu ujao.

"Tumeachana na kocha Olaba kwa amani kabisa hatuna matatizo nae, tunamtakia kila la kheri aendako, tuliishinae vizuri lakini mabadiliko tuliyofanya tumeona haina budi kumuweka pembeni," alisema Masau.

Olaba alichukua mikoba uliyoachwa na kocha Boniface Mkwasa ambaye alikwenda kujiunga na timu ya Yanga katika msimu wa 2014/15 na kufanikiwa kukamata nafasi ya tano katika msimao wa ligi kuu Tanzania bara baada ya kujikusanyia alama 35.

Post a Comment

 
Top