BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
UONGOZI wa klabu ya Mbeya City umemuongeza kandarasi ya mwaka mmoja beki wake Haruna Shamte kwa ajili ya kuendelea kuwatumikia Wagonga nyundo hao.

Shamte ambaye aliwahi kuichezea timu ya Simba ni miongoni wachezaji wenye uzoefu ndani ya kikosi hicho mpaka kufikia kocha Mzambia Kinnah Phiri kuutaka uongozi kumuongezea kandarasi ya mwaka mmoja.

Katibu mkuu wa Mbeya city Emmanuel Kimbe ameithitishia BOIPLUS kuwa beki huyo mwenye uwezo wa kucheza nafasi zote za ulinzi amesaini mkataba wa mwaka mmoja mchana huu kwa ajili ya kuendelea kuwatumikia vigogo hao wa jiji la Mbeya.

"Ni kweli amesaini kandarasi ya mwaka mmoja kuendelea kusalia kwetu, na mchana wa leo kila kitu kilienda sawa," alisema Kimbe.

City wataanzia ugenini katika mechi yao ya ufunguzi ambapo watasafiri hadi mkoani Kagera kukipiga na Wanankulumbi katika dimba la Kaitaba Agosti 20.

Msimu uliopita kikosi hicho hakikuwa katika ubora ambao mashabiki wengi waliuzoea baada ya kuondokewa na nyota wake kadhaa kama Deus Kaseke na Peter Mwalyanzi.

Jiji la Mbeya linawakilishwa na timu mbili katika ligi kuu ya Vodacom  ambazo Wajelajela Tanzania Prisons na Mbeya City.

Post a Comment

 
Top