BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
UONGOZI wa klabu ya Simba umepanga maadhimisho ya timu hiyo kuzinduliwa na mkutano mkuu wa wanachama utakaofanyika katika bwalo la maofisa wa Polisi Oysterbay Jumapili Julai 31.

Simba imejiwekea utaratibu wa kila mwaka ifikapo Agosti 8 kuadhimisha siku yao kwa kufanya shughuli mbali mbali zikiwemo kutambulisha wachezaji pamoja na jezi zitakazotumika msimu mzima.

Rais wa klabu hiyo Evans Aveva amewaambia waandishi wa habari kuwa msimu huu maadhimisho hayo yameboreshwa kulinganisha na miaka iliyopita ili kuwapa nafasi wapenzi na wanachama wengi kujitokeza kwa wingi kushiriki.

Katika siku hiyo Simba itacheza mechi ya kirafiki na timu ya Interpool toka nchini Angola kwa ajili ya kukipima kikosi chake kabla ya kuanza kwa mikikimikiki ya ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara.

"Wiki ya Simba itafunguliwa na mkutano mkuu ambao tutajadiliana mambo mengi kuhusu mustakabali wa timu ambapo wanachama watapata fursa ya kutoa mapendekezo kuhusu uendeshwaji wa klabu," alisema Aveva.

Aveva alisema pia kuanzia Agosti mosi hadi siku ya kilele klabu hiyo itafanya shughuli mbali mbali za kijamii kama kuwatembelea wachezaji wa zamani wa timu hiyo na kuchangia damu katika hospitali ya taifa Muhimbili.

Aidha Rais huyo amewataka wanachama ambao bado hawajalipia kadi zao wafanye hivyo haraka ili waweze kupata nafasi ya kushiriki mkutano huo utakaotoa dira ya maendeleo ya klabu hiyo.

"Niwaombe wanachama wetu popote walipo kulipia kadi zao za uanachama ili wapate nafasi ya kushiriki katika mkutano huo" alimalizia Aveva.

Post a Comment

 
Top