BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar

UONGOZI wa klabu ya Simba umeziita mezani timu zinazohitaji saini ya beki wake Hassani Isihaka kutokana na kutokuwepo katika mipango yao ya msimu ujao.

Beki huyo amebakisha mkataba wa miaka miwili na Wekundu hao baada ya kusaini kandarasi ya miaka mitatu mwaka jana ambapo mpaka sasa ametumikia mwaka mmoja huku akitakiwa atafute pa kutokea ili kuepuka kukaa bechi katika kikosi cha Mcameroon Joseph Omog.

Rais wa Simba Evans Eveva ameiambia BOIPLUS kuwa ameitaka timu iliyopanda daraja msimu huu African Lyon kuandika barua endapo wanamuhitaji ili wamtoe hata kwa mkopo.

"Isihaka bado ni mchezaji wetu ana mkataba wa miaka miwili umebaki, lakini kwa mahitaji ya kikosi msimu ujao anaweza asipate nafasi kwahiyo kama kuna timu inahitaji hudumu yake sisi tuko tayari," alisema Aveva.

Katika siku za karibuni kumekuwa na uvumi wa beki huyo kusaini kandarasi na timu ya Ndanda FC ya mkoani Mtwara lakini uongozi wa klabu hiyo ulikanusha vikali tetesi hizo.

BOIPLUS ilimtafuta Katibu mkuu wa Ndada Selemani Kachele kuthibitisha uvumi huo ambapo alisema, "hatujamsajili Isihaka wala hatujafanya makubaliano yoyote nae kuhusu usajili wetu wa msimu huu tutaweka wazi kila kitu muda ukifika."

Kikosi cha Ndanda kinatarajia kuingia kambini Julai 17 jijini Dar es Salaam chini ya kocha Malale Hamsini tayari kwa maandalizi ya ligi kuu msimu mpya.

Post a Comment

 
Top