BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu, Dar
KLABU ya Simba ipo katika mchakato wa kukijenga kikosi chao cha msimu ujao, na baada ya kuachana na mganda Hamis Kiiza wekundu hao wameamua kuyasaka mabao kwa mshambuliaji wa Azam FC Ame Ally 'Zungu' kwa kufanya mazungumzo na timu hiyo ili atue kwa mkopo.

Ame alishindwa kupata namba ya kudumu katika kikosi cha Azam msimu uliopita huku ikionekana pia anaweza asiwe na nafasi katika kikosi cha kocha Zeben Hernandez hali iliyopelekea kuhusishwa na mpango wa kutolewa kwa mkopo.

Kiongozi mmoja mwenye ushawishi mkubwa ndani ya Simba ameiambia BOIPLUS kwa masharti ya kutotajwa jina lake mtandaoni kuwa mazungumzo yamefikia pazuri na muda wowote kuanzia sasa mshambuliaji huyo atakuwa mikononi mwa Wekundu hao akitokea Chamazi.

"Tupo kwenye mazungumzo ya mwisho na Azam Mungu akipenda wiki ijayo Ame atakuwa ameshakamilisha usajili wa kujiunga nasi," alisema kiongozi huyo.

Kwa upande wake Mtendaji mkuu wa Azam Saad Kawemba alisema hawezi kuelezea sana  suala la Ame kwavile wamepokea maombi mengi toka kwa timu zinazoshiriki ligi kuu kuwahitaji wachezaji wao kwa mkopo na bado wanapitia maombi hayo ili kujiridhisha kabla ya kutoa maamuzi.

"Maombi ni mengi lakini bado tunayafanyia tathimini kabla ya kutoa maamuzi siku chache zijazo," alisema Kawemba.

BOIPLUS ilimtafuta Ame kutaka kujua kama ana taarifa zozote kuhusiana na uhamisho huo wa mkopo kuelekea Simba lakini simu yake iliita bila kupokelewa. Hata hivyo rafiki zake wa karibu waliupasha mtandao huu kuwa alipewa machaguo mawili na yeye amechagua kujiunga na Wekundu wa Msimbazi.

Post a Comment

 
Top