BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar

KIKOSI cha timu ya Simba kimendoka mchana wa leo kuelekea mkoani Morogoro kwa ajili ya kuweka kambi kabla ya kuanza kwa mikikimikiki ya ligi kuu Tanzania bara mwezi ujao.

Rais wa klabu hiyo Evans Aveva amesema wameamua kuwaita wachezaji wote klabuni hapo ili kuwatambulisha kwa viongozi kabla ya kwenda kuweka kambi tayari maandalizi ya msimu ujao.

"Tumewaita kuwatambukisha wachezaji wetu wa kigeni pamoja na wazamani kwa uongozi kabla ya timu kwenda Morogoro" alisema Aveva.

Wachezaji wa Wekundu hao waliwasili kwa makundi katika jengo la klabu yao na kukutana na viongozi wa timu na kufanya kikao cha siri ambapo hakukuruhusiwa wanahabari kuingia ndani ingawa BOIPLUS inafahamu kuwa kumefanyika dua ya kuwaiombea timu hiyo.

Wachezaji wapya Mousa Ndusha, Janvier Bukungu wakiongozwa na golikipa Vincent Agban ndiyo walikuwa wakwanza kuwasili klabuni hapo huku wakilakiwa na baadhi ya wapenzi na wanachama wa timu hiyo ambao wameonesha imani kubwa juu ya wanandinga hao.

Jana Simba ilikamilisha usajili wa kiungo Shiza Kichuya kutoka Mtibwa Sugar na kuungana na wachezaji wengine Mohamed Ibrahim na Muzamir Yassini waliokuwa wakiwatumikia wakata miwa hao toka Morogoro.

Simba inayonolewa na kocha Mcameroon Joseph Omog akisaidiwa na Jackson Mayanja imepania kufanya vizuri msimu unaokuja ili kurejesha makali yake yaliyopotea kwa miaka minne na kuwafurahisha wapenzi wa timu ambao wamekata tamaa kutokana na mwenendo mbovu wa timu.

Habari za ndani toka Simba zinasema mshambuliaji Mrundi Laudit Mavugo atatua kesho nchini tayari kujiunga na kambi ya timu hiyo mkoani Morogoro.

Post a Comment

 
Top