BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu,Dar
SIKU moja baada ya mshambuliaji Laudit Mavugo raia wa Burundi kutimkia nchini Ufaransa kufanya majaribio kwenye klabu ya Tours inayoshiriki ligi daraja la pili, Uongozi wa klabu ya Simba umemfuta katika mipango yake ya baadae.

Mavugo amekuwa akihusishwa kujiunga na Wekundu hao tangu msimu uliopita huku taarifa zikisema  tayari alishachukua fedha nusu za kujiunga na miamba hiyo mwaka jana ambazo ni Dola 10,000.

Makamu wa Rais wa klabu hiyo Godfrey Nyange 'Kaburu' ameiambia BOIPLUS kuwa wameamua kuachana mshambuliaji huyo ambaye amekuwa akiwapiga dana dana tangu mwaka jana na kukwamisha mipango yao ambapo sasa ametimkia nchini Ufaransa.

"Tumesikia kwenye vyombo vya habari kuwa ameenda Ufaransa siku ambayo ilikuwa aje nchini kujiunga na Simba kwahiyo hatuna haja ya kufuatilia mtu asiye na msimamo tutapata wachezaji wazuri hata zaidi yake" alisema Kaburu.

Makamu huyo alisema pia wanaendelea kupokea wachezaji wa kimataifa kwa ajili ya majaribio na watakaofaulu watasaini kandarasi ya kujiunga na Wekundu wa msimbazi.

"Bado wachezaji wa kimataifa wataendelea kuja kufanya majaribio chini ya kocha Joseph Omog atakayefaulu tutamsajili moja kwa moja" alisema Kaburu.

Kikosi cha Simba kipo mkoani Morogoro wiki ya pili sasa kikijifua kwa ajili ya msimu mpya wa ligi unaotarajiwa kuanza mwezi ujao.

Post a Comment

 
Top