BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
MSHAMBULIAJI wa Simba aliyekuwa akichezea Kagera Sugar kwa mkopo msimu uliopita Mbaraka Yusuph ameugomea uongozi wa klabu hiyo kurejea Msimbazi baada ya kushindwa kumlipa stahiki zake.

Mshambuliaji huyo ambaye aliifungia Kagera magoli nane msimu uliopita anatakiwa kurejea kwa Wekundu hao baada ya kufanya vizuri akiwa na Wanankulumbi na sasa waajiri wake timu ya Simba wamekoshwa na uwezo aliouonyesha.

Mbaraka ambaye kwa sasa yupo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mazungumzo na viongozi wa Simba ameiambia BOIPLUS kuwa  kipindi chote ambacho alikuwa Kagera kwa mkopo hajawahi kulipwa chochote na Wekundu hao.

"Sijawahi kulipwa chochote na Simba kipindi chote nilichokuwa Kagera wameniita wanataka nirudi ila mpaka wanihakikishie stahiki zangu," alisema Mbaraka.

Mtandao huu ulifanya jitihada za kuwatafuta viongozi wa Simba ili kuweza kuzungumzia madai ya mchezaji huyo lakini hakuna aliyepokea simu.

Mbaraka alikuwa miongoni mwa wachezaji walioisaidia Kagera kusalia katika ligi kuu baada ya kuibuka kinara wa magoli ndani ya kikosi hicho kilichokuwa kikinolewa na kocha Adolf Rishard.

Msimu mpya wa ligi utakaoanza Agosti 20 na kikosi cha Kagera kitakuwa chini ya kocha Meck Mexime ambaye msimu uliopita alikuwa Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro.

Post a Comment

 
Top