BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu
KUELEKEA mkutano mkuu wa wanachama wa Simba uliopangwa kufanyika Julai 31, sehemu kubwa ya wanachama wa klabu hiyo wamekuwa wakihimizana kufanya mabadiliko ambayo yataipeleka katika mfumo wa Hisa.

BOIPLUS ilifanikiwa kuunasa ujumbe mmoja ambao umesambazwa sana wenye mitandao ya kijamii unaowahamasisha wanachama hao kuhudhuria kwa wingi kwa lengo la kwenda kufanya maamuzi ya kihistoria.

Huu hapa ujumbe wa Geffrey Kapyata Shimwela mwanachama wa Simba mwenye kadi namba 8379.


ASSALAM ALEYKUM NDUGU ZANGUNI.

BWANA YESU ASIFIWE.

Awali ya yote ashakuriwe Mwenyezi Mungu aliye mwingi wa rehema.

Ule wakati wa Wanasimba kutembea vifua mbele kuvaa jezi zetu mpaka sehem za makazi na starehe sasa umewadia. 

 Mwanasimba popote ulipo ewe mwanachama amini sasa Julai 31 siku ya mkutano mkuu wa wanachama wa Simba ni siku ya kuikwamua Simba kutoka hapa tulipokwama kwa miaka mingi kwenda katika dunia ya usasa, dunia ya 'kidigitali'

Ni mkutano mkuu wa kihistoria katika Klabu ya Simba. Tutumie nafasi hiyo adhimu katika kuchagua mfumo wa kibiashara/wa kisasa kama mfumo ufaao kuiendesha 'Simba Sports Club'. Ni mfumo utakaotutoa huku tulikofeli miaka mingi (mfumo wa kadi) na kuja katika mfumo wa HISA ambao unatoa nafasi kwa wawekezaji kuwekeza pesa zao ndani ya klabu yetu pendwa ya Simba.

Ni mfumo wa dunia ya kileo ya michezo, klabu nyingi zenye kuendelea na kufanikiwa zinatumia mfumo huu wa kibiashara,  mfumo unaowezesha timu kuwa na faida zifuatazo;

1. Kujiendesha pasipo kumtegemea mtu 
2. Kuwa na miundombinu yake kama uwanja, maduka ya jezi nk.
3. Usimamizi mzuri wa masuala ya fedha
4. Wawekezaji kupata gawio lao baada ya faida kupatikana

Ewe mwanasimba ni nafasi yako sasa kuwa miongoni mwa wanachama wengi watakaoandika historia ya kuiongoza klabu yao kwenda katika mfumo wa kisasa mfumo wa kibiashara mfumo wa kujiendesha na kujitegemea na kuwa miongoni mwa klabu za kisasa barani Afrika. 

Mwanachama wa simba jiandae kimwili na kiakili kufanya maamuzi sahihi katika mkutano wa kihistoria. Badala ya kusikiliza maneno ya vijiwe tu basi ni wakati wako sasa mwanasimba kupata madarasa huru ya elimu juu ya uwekezaji ufaao katika klabu yetu ili upate kwenda kuamua kilicho sahihi zaidi kwa mstakabli wa club yako na sio mstakabali wa matumbo ya wachache. 

Upotoshaji
 Mwanasimba uliye na mapenzi mema na klabu yako, Mwenye kuitakia heri na mafanikio club yako yazibie masikio maneno yanayotoka kwa watu wenye maslahi binafsi wasemao Simba  inauzwa. Ni upotoshaji mkubwa unaoenezwa na wale wasioitakia mema simba kwa maslahi yao binafsi na kwa maslahi ya wapinzani wetu wakubwa katika soka nchini. 

Usiache bahati hii ya kihistoria ikupite. Tembea kifua mbele, unguruma popote kuwa wewe unataka mabadiliko ya kiuendeshaji ndani ya Simba na upo tayari kwenda kupiga kura Julai 31, kura ya kuidhinisha mfumo wa biashara mfumo wa kisasa kama mfumo ufaao kuiendesha Simba yenye hadhi ya kuitwa Taifa kubwa.

MOLA JALIA WANACHAMA WA SIMBA SPORTS CLUB

MUNGU IBARIKI SIMBA SPORTS CLUB.
Post a Comment

 
Top