BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu, Dar
KIUNGO wa zamani wa timu ya Yanga Salum Telela amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia timu ya Ndanda FC baada ya kandarasi yake kwisha na mabingwa hao.

Mkataba wa Telela na Yanga ulimalizika mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kuisaidia timu hiyo kutetea ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara pamoja na kuchukua  ubingwa wa kombe la FA.

Telela ameiambia BOIPLUS kuwa amesaini mkataba na Ndanda kutokana na makubaliano baina yao kwenda vizuri licha ya kupokea ofa nyingi kutoka timu zinazoshiriki ligi kuu.

"Nimesaini mwaka mmoja Ndanda, hivyo msimu ujao nitawatumikia baada ya kufikia makubaliano ya pande zote mbili," alisema Telela.

Kwa upande wake katibu mkuu wa Ndanda Selemani Kuchele alisema wamemsajili kiungo huyo kutokana na uwezo aliokuwanao ambao utasaidia kuimarisha timu hasa kutokana na uzoefu wake kwenye ligi.

"Tumemsajili Telela kwa mkataba wa mwaka mmoja tunaamini bado ni mchezaji mzuri ambaye atakuwa na msaada mkubwa sana kwetu," alisema Kuchele.

Timu hiyo bado ipo kwenye mkakati wa kutafuta kocha mpya baada ya aliyekuwa mwalimu wao Malale Hamsini kutimkia JKT Ruvu.

Post a Comment

 
Top