BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
Yusuf Mgwao kushoto akiwa Friends Rangers, kulia ni kinda Cliff Buyoya ambaye amesajiliwa na KMC

WACHEZAJI wa Kitanzania wametakiwa kuwaheshimu makocha wazawa kama wa kigeni ili waweze kufanikiwa kufika mbali katika medani ya Soka.

Makocha wakigeni wamekuwa wakiheshimiwa zaidi ukilinganisha na wazawa hali ambayo haileti picha nzuri katika maendeleo ya mpira wa miguu kote duniani.

Kauli hiyo imetolewa na winga wa zamani wa timu ya Simba aliyejiunga na Majimaji ya Songea Yusuph Mgwao alipokuwa akizungumza na BOIPLUS kuhusu kusajili wake na 'Wanalizombe' hao.

Mgwao amejiunga na Majimaji akitokea Friends Rangers huku uzoefu wake ukitarajiwa kuwa msaada mkubwa kutokana na kuwa kiongozi mzuri ndani ya uwanja.

"Makocha wazawa hawapewi thamani kubwa kulinganisha na wageni ila hayo ni makosa makubwa kwakua linaweza kudumaza soka sababu wako wengi kuliko wazungu," alisema Mgwao.

Mgwao amewataka wachezaji, benchi la ufundi, viongozi, wanachama pamoja na mashabiki wa timu hiyo kuwa pamoja katika kila hatua ili kuifanya timu yao kufanya vizuri msimu mpya unaotarajiwa kuanza Agosti 20.

Aidha winga huyo alisema ligi itakuwa ngumu kutokana na timu nyingi kufanya maandalizi mazuri kuelekea msimu ujao kitu ambacho kinatia hamasa kwa wachezaji.

Mgwao ambaye amekosekana katika ligi kuu misimu mitatu amejipanga kikamilifu kurejesha makali yake na uzoefu baada ya msimu uliopita kuitumikia timu inayoshiriki ligi daraja kwanza Friends.

" Nimejipanga vizuri kurudi tena ligi kuu japokuwa kuna changamoto nyingi ila nitatumia kipaji na uzoefu nilionao kuisaidia Majimaji," alisema Mgwao.

Majimaji inanolewa na kocha Hassani Banyai aliyechukua mikoba ya Kali Ongola aliyemaliza mkataba na Wanalizombe hao.

Post a Comment

 
Top