BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda, Dar
HAFLA ya kukabidhi tuzo za ligi ya Vodacom msimu wa 2015/16 zimemalizika muda mfupi uliopita katika Hoteli ya Double Tree By Hilton huku tuzo 13 zikitolewa kwa washindi wa nyanja mbalimbali.

Yanga ilikabidhiwa zawadi ya Ubingwa walioutwaa huku nafasi ya pili ikienda kwa Azam FC mbele ya Simba ambayo imeambulia zawadi ya mshindi wa tatu. Timu ya jeshi la Magereza, Prisons ya Mbeya  ambayo ilionyesha uwezo mkubwa msimu huo ilikamata nafasi ya nne.

Kwa upande wa mwamuzi bora, Ngole Mwangole alitwaa tuzo hiyo akiwapiku wezake wawili aliokuwa akiwania nao. Wakati huo huo Mtibwa Sugar ya Morogoro ilitajwa kama timu yenye nidhamu zaidi.


Mshambuliaji kutoka Burundi, Amissi Tambwe wa Yanga alitwaa tuzo ya mfungaji bora huku klabu hiyo ikitoa pia Kocha Bora, Hans Van Pluijm.

Kipa namba moja wa Azam Fc, Aishi Manula alitangazwa kuwa kipa bora wakati tuzo ya bao bora ilienda kwa Ibrahim Ajibu wa Simba.

Safari hii tuzo ya mchezaji bora wa kigeni imetua kwa kiungo wa Yanga Thaban Kamusoko huku kinda Mohamed Hussein 'Zimbwe' akiweka kapuni tuzo ya mchezaji bora chipukizi.

Tuzo ambayo ilikuwa na mvuto zaidi huku ikisubiriwa kwa hamu na wadau wa soka ni ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom 2015/16 ambayo ilitua kwa beki wa kulia wa Yanga, Juma Abdul ambaye alikuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo kwenye msimu uliopita.

Post a Comment

 
Top