BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar

KIKOSI cha mabingwa wa ligi kuu Tanzania bara timu ya Yanga kipo kamili kwa ajili ya mchezo wao wa kombe la shirikisho utaopigwa kesho dhidi ya Medeama toka Ghana katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga itawakosa wachezaji watatu ambao hawapo kambini kutokana na majeruhi kama vile Gofrey Mwashiuya, Deus Kaseke huku Haji Mwinyi akiwa na kadi nyekundu aliyoipata katika mchezo dhidi ya Mo Bejaia.

Daktari wa timu hiyo Edward Bavu ameiambia BOIPLUS kuwa ukiwatoa wachezaji hao watatu wengine wote wapo timamu kwa ajili ya mchezo huo ambao wanatakiwa kushinda ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele.

"Tambwe (Amissi) ndiyo alikuwa na malaria na jana alijiunga na wenzie mazoezini, kwa sasa tunamshukuru Mungu kikosi kipo vizuri na leo walifanya mazoezi asubuhi hatukupata majeruhi yeyote," alisema Bavu.

Yanga watatakiwa kuibuka na ushindi katika mchezo huo kwakua wamebakiwa na mchezo mmoja nyumbani dhidi ya Mo Bejaia huku wakitakiwa kusafiri hadi Lubumbashi kuwakabili vinara wa kundi hilo TP Mazembe wenye alama sita.

Tayari mabingwa hao kupitia kwa kaimu katibu mkuu wao Deusdedith Baraka wametangaza viingilio vya mchezo huo ambapo kiingilio cha chini kitakuwa shilingi 3000 na cha juu kikiwa 15,000.

Post a Comment

 
Top