BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma,Chamazi
TIMU ya Azam FC imebanwa mbavu baada ya kulazimishwa sare ya goli 1-1 na African Lyon katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom uliopigwa kwenye uwanja Azam Complex hapa Chamazi.

Mchezo huo ilikuwa wa kasi huku timu zote zikishambuliana kwa zamu lakini Lyon walikuwa bora zaidi huku wakionekana kama wao ndiyo wenyeji wa mechi hiyo.

Dakika ya 46 Lyon walipata goli kupitia kwa Mayanja Abdul baada ya kupiga kona iliyotinga moja kwa moja nyavuni na kumuacha kipa Aishi Manula akichupa bila mafanikio.

Kuingia kwa goli hilo kuliwaamsha Azam na kuanza kushambulia kama nyuki lango la Lyon lakini umakini wa walinzi waliokuwa chini ya Hamadi Waziri uliwafanya kukosa ubunifu.

Wachezaji wawili wa  Lyon walionywa kwa kadi ya njano na mwamuzi Israel Nkongo kwa kuchelewesha mchezo.

Dakika ya 90 nahodha John Bocco 'Adebayor' aliisawazishia Azam baada ya kuwazidi ujanja mabeki Lyon kabla ya kumchambua mlinda mlango Youthe Rostand.

Azam iliwatoa Frank Domayo,Shabani Chilunda na Ismail Gambo na nafasi zao kuchukulia na Michael Boloue, Fransico Zekumbariwa pamoja na Mudathir Yahaya. Lyon ilimpumzisha Omari Abdallah na kumuingiza Hilal Hassan.

Baada ya kumalizika kwa mchezo huo mchezaji Hamad Waziri alioneshwa kadi nyekundu baada ya kumzonga mwamuzi kutokana na kutoridhishwa na maamuzi.

Post a Comment

 
Top