BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu,Chamazi
TIMU ya Azam FC imelazimishwa sare ya goli 1-1 na Maafande wa JKT Ruvu katika mchezo wa kujipima nguvu uliofanyika katika uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Mchezo huo ni maandalizi ya timu zote mbili kujiweka sawa kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara utakaoanza Agosti 20.

Azam ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata goli kwa mkwaju wa penalti liliofungwa na beki Agrey Morris dakika ya 44 baada ya Rashidi Juma kuunawa mpira katika eneo la hatari.

Goli hilo lilidumu kwa dakika 20 tu kwani Hasani Matalema alisawazisha baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa mshambuliaji mpya wa Maafande hao Atupele Green na kuwazidi ujanja mabeki wa Azam.

Katika mchezo huo ulihudhuriwa na mashabiki wengi kutokana na kutokuwepo kwa kiingilio hali iliyopelekea watu wengi kujitokeza kwa wingi.

Azam wamerejea wiki iliyopita kutokea visiwani Zanzibar walipoweka kambi ya wiki mbili kwa ajili ya maandalizi ya ligi na mchezo wa ngao ya Hisani utakaochezwa Agosti 14 dhidi ya Yanga.

Post a Comment

 
Top