BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
Mlinzi wa kulia wa URA, Julius Ntambi

BEKI wa kulia wa Simba Janvier Bokungu raia wa DR Congo huenda akakatwa katika kikosi hicho baada ya benchi la ufundi pamoja na viongozi wa Simba kutoridhishwa na kiwango chake na badala yake nafasi hiyo inatajwa kuchukuliwa na Julius Ntambi wa URA ya Uganda.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo ambazo BOIPLUS imezinasa zinasema kwamba mazungumzo ya awali na beki huyo wa timu ya taifa ya Uganda 'The Cranes' yameanza kufanywa na endapo yatakwenda vizuri basi Bokungu atafungashiwa virago.

Tangu awali kumekuwepo na taarifa kwamba kiwango cha Bokungu hakikuwaridhisha wengi ndani ya Simba ambapo walifikia hatua ya kumpa mkataba wa miezi sita huku wakiwa wanaendelea kutafuta mbadala wake.

"Bokungu bado kiwango chake si cha kucheza Simba hii yenye ushindani na ndiyo maana tulimpa mkataba wa miezi sita na sasa kuna mazungumzo yanayoendelea na beki wa URA endapo tutakubaliana basi tutaachana na Bokungu," alisema kiongozi huyo.

Ntambi mwenye miaka 24 ndiye aliifungia URA bao la kwanza katika mchezo wa Fainali ya kombe la Mapinduzi dhidi ya Mtibwa mwezi Januari.

Simba bado wana nafasi ya kufanya marekebisho kwa wachezaji wao wa kigeni kwani dirisha la usajili kwa upande wa wachezaji hao halijafungwa.

Post a Comment

 
Top