BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu, Dar
LICHA  ya kukosekana  kwa mshambuliaji wao hatari Donald Ngoma kikosi cha timu  Yanga kipo kamili 'gado' kuwavaa waarabu wa Algeria, Mo Bejaia katika mchezo wa marudiano wa kombe la shirikisho barani Afrika utakaopigwa katika Uwanja wa Taifa Agosti 13.

Yanga itashindwa kumtumia  mfumania nyavu huyo aliyefunga mabao manne mpaka sasa katika michuano hiyo  kutokana na adhabu ya kadi Tatu za njano ambayo kwa mujibu wa  kanuni za Shirikisho la Soka Afrika CAF mchezaji anapaswa kukosa mchezo unaofuata.

Akiongea na BOIPLUS leo kocha msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi alisema kila mchezaji ana umuhimu wake kikosini ila Ngoma alihitajika zaidi kutokana uzoefu wake katika mechi za kimataifa na umahiri wa kufunga.

"Yanga tumesajili wachezaji 30 kila mchezaji ana umuhimu wake kwahiyo pengo la Ngoma litazibwa na mtu mwingine ambae mwalimu ataona anafa," alisema Mwambusi.

Aidha mabingwa hao sasa wana uhakika wa kumtumia  winga wake Deus Kaseke ambaye amepona majeraha yaliyotokana  na ajali ya pikipiki maarufu kama bodaboda.

Kikosi cha Yanga kinaendelea na mazoezi yake katika uwanja wa Gymkana kwa maandalizi ya mtanange huo ambao watalazimika kushinda ili kufufua matumaini ya  kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Post a Comment

 
Top