BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
PAZIA la ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara linafunguliwa kesho ambapo timu 12 zitashuka dimbani huku mbili zikicheza siku ya Jumapili. Mabingwa watetezi Yanga wao wataanza Agosti 31 kutokana na mchezo wao wa kukamilisha ratiba wa kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya TP Mazembe utakaochezwa Jumanne ijayo.

Katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Wekundu wa Msimbazi Simba wakiwa na nyota kama Laudit Mavugo, Shiza Kichuya na Ibrahim Ajib  watashuka dimbani kuwakaribisha Ndanda FC katika mechi ambayo inawakutanisha makocha wawili ambao hawakuwa na vikosi hivyo msimu uliopita.

Simba wapo chini ya kocha Joseph Omog raia wa Cameroon ambaye amekisuka kikosi hicho kinachoonekana kina mabadiliko makubwa ya kiuchezaji kulingana na wachezaji waliowasajili huku Hassani Banyai akichukua nafasi ya Hamsini Malale kuwanoa wanakuchele hao ambao wamepania kufanya makubwa msimu huu.

Mchezo mwingine utakuwa katika uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga ambapo Kagera Sugar itawakaribisha Mbeya city katika mchezo utakaovuta hisia za wapenzi wa soka baada ya kocha Meck Mexime kuchukua mikoba ya kuwanoa Wanankulumbi hao huku Kinnah Phiri akiwa na Wagonga Nyundo wa jiji la Mbeya.

Mtanange mwingine utakuwa katika uwanja wa Manungu mkoani Morogoro ambapo Mtibwa Sugar itawakaribisha Ruvu Shooting waliopanda daraja msimu huu huku wakiapa kuwa wamedhamiria kunyakua ubingwa wa ligi kuu msimu wa 2016/17 "Tumejipanga kunyakua ubingwa msimu huu na tutawashangaza wengi" alisema Ofisa Habari wa Ruvu Masau Bwire.

Mechi nyingine zitakuwa kati ya Majimaji vs Tanzania Prisons, Stand United vs Mbao FC, Toto African vs Mwadui inayonolewa na kocha mbwatukaji Jamhuri Kihwelo 'Julio'.

Keshokutwa Azam FC watakuwa katika uwanja wa Chamazi Complex kuwakabili African Lyon ambao nao wamepanda ligi msimu baada ya kukosa kwa misimu miwili mfululizo.Wana ramba ramba wana nafasi ya kushinda baada ya kuwafunga Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii Jumatano iliyopita likiwa na taji la kwanza kwa kocha Mhispaniola Zeben Hernandez.

Post a Comment

 
Top