BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
MAAFANDE wa JKT Ruvu kesho watashuka dimbani kumenyana na Azam FC katika mchezo wa kujipima nguvu utakaofanyika kwenye uwanja wa Chamazi Complex saa 10 jioni huku wakitamba kutisha katika mchezo huo.

Maafande hao ambao wanafanya mazoezi katika uwanja wa JKT Mbweni ambapo ndio wameweka kambi kwa ajili ya kujiwinda na michuano ya ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara itakayoanza Agosti 20 utakuwa ni mchezo wao wa kwanza mkubwa wa kujipima nguvu.

Ofisa Habari wa klabu hiyo Constantine Masanja ameiambia BOIPLUS kuwa wachezaji wote wako vizuri na wanasubiri kwa hamu kubwa kufunguliwa kwa pazia la ligi ili waweze kuwaonesha wapenzi wa timu hiyo jinsi ya kusakata kandanda.

"Wachezaji wote wako timamu kwa ajili ya mchezo wetu na Azam hiyo kesho na wameahidi kuibuka na ushindi ili kuziwashia taa ya nyekundu timu zinazoshiriki ligi kuu msimu ujao,"alisema Masanja.

Kikosi hicho cha Maafande hao kipo chini ya mwalimu msaidizi Azishi Kondo huku wakimsubiri kocha mkuu Malale Hamsini ambaye muda wowote atajiunga nao baada ya kumaliza kozi ya ukocha wa leseni A hatua ya kwanza inayotolewa na shirikisho la mpira barani Afrika CAF.

Msimu uliopita Maafande hao walikuwa wakinolewa na kocha Abdallah Kibaden 'Mputa' ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa ufundi wa kikosi hicho kwa sasa.

Post a Comment

 
Top