BOIPLUS SPORTS BLOG

LUBUMBASHI, DR Congo
TIMU ya Yanga imemaliza michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya TP Mazembe kwa kuambulia kichapo cha mabao 3-1 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Stade de Mazembe.

Mchezo wa awali uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Yanga ilikubali kufungwa goli 1-0 dhidi ya mabingwa hao wenye historia kubwa kwenye medani ya soka barani Afrika.

Jonathan Bolingi aliwapitia wenyeji goli la ufunguzi dakika ya 28 baada ya kupokea pasi toka kwa Deo Kanda aliyewahadaa mabeki wa Yanga.

Yanga walicheza muda mrefu wakiwa pungufu baada ya beki Vicent Andrew kuoneshwa kadi nyekundu dakika ya 30 baada ya kumchezea rafu Rainford Kalaba.

Kalaba alifunga magoli mengine mawili dakika ya 55 na 63 na kuwafanya Yanga kutoka vichwa chini baada ya kumaliza hatua ya makundi wakiwa na alama nne na kuburuza mkia kwenye kundi hilo.

Mshambuliaji Amissi Tambwe aliipatia Yanga goli la kufutia machozi dakika ya 74 baada ya kumalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Haruna Niyonzima ambao uligonga mwamba kabla ya kumkuta mfungaji.

Mazembe wamemaliza hatua hiyo wakiwa vinara wa kundi A baada ya kujikusanyia alama 13, wakifuatiwa na Medeama 8,Bejaia 5 na wa mwisho ni Yanga wenye pointi 4.

Msimamo huo ni kabla ya matokeo ya Medeama na Bejaia ambao wapo dimbani sasa hivi.

Post a Comment

 
Top