BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
MWADUI FC ilimsajili kiraka wa Ndanda FC, William Lucian 'Gallas' kwa mkataba wa mwaka mmoja na baadae ikafahamika kuwa tayari nyota huyo alisaini mkataba mpya na timu yake ya zamani kosa ambalo limemfanya afungiwe mwaka mmoja kucheza soka popote.

Viongozi wa Ndanda ya Mtwara wameweka wazi kuwa mchezaji huyo hawezi kucheza Mwadui kwani ni mali yao na tayari pengo lake lilionekana katika mechi yao ya ligi dhidi ya Simba ambapo walifungwa bao 3-1, mechi iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Gallas alisaini mkataba na Mwadui na kujiunga nayo ingawa imeelezwa kuwa leo alitarajiwa kurejea Dar es Salaam ili kuja kumaliza tatizo lake hilo ambapo anapaswa kuchagua sehemu moja pekee ingawa sheria inaweza kumuonea huruma na kumrudisha kucheza Ndanda FC.

Katibu Mkuu wa Ndanda, Seleman Kachele alifafanua kuwa; "Gallas ni mchezaji wetu kwani alisaini mkataba mpya wa mwaka mmoja, Mwadui walifanya kosa kubwa kuzungumza na mchezaji ambaye ana mkataba, walitakiwa kutufuata kwanza jambo ambalo halijafanyika hadi sasa na hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika kati yetu na Mwadui.

"Ili acheze yeye ndiye anayepaswa kuandika barua ya maelezo kwenda TFF ambao ndiyo waliotoa adhabu hiyo, kuna makosa mengi yamefanyika juu yake, pia mkataba wake uko wazi kwamba timu inayotaka kuvunja mkataba inapaswa kulipa Sh 15 milioni ila kwa hapa ilipofikia Mwadui watapaswa kutulipa Sh 50 milioni kwa makosa hayo," alisema Kachele.

Kwa upande wa Katibu mkuu wa Mwadui, Ramadhan Kilao alikiri kutomalizana na Ndanda ingawa alisema mazungumzo ya awali yalifanyika na ndiyo maana beki huyo alikuwepo kambini kwao Shinyanga.

"Tuliwaomba tulipe fedha ambayo wamempa, walikubali lakini tulishangaa nao wamepeleka jina lake TFF, hivyo tutazungumza nao kuona ni jinsi gani Gallas anaweza kucheza na kuwalipa fedha ambayo tulikubaliana nao ndipo twende TFF kutoa maelezo," alisema Kilao ingawa kauli yake ilipingwa vikali na viongozi wa Ndanda

Post a Comment

 
Top