BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Simba Paul Kiongera anayechezea AFC Leopards amewashukuru mashabiki wa klabu ya Simba kwa upendo waliomuonyesha katika mchezo  ambao walilala magoli 4-0 mbele ya Wekundu wa Msimbazi.

Kiongera ambaye alikuwa akishangiliwa na mashabiki wa timu hiyo kila akigusa mpira alisema amefurahishwa  kwa kitendo hicho huku pia akishukuru kwa mapokezi aliyoyapata toka kwa Wekundu hao.

Katika Maadhimisho kama hayo mwaka jana Kiongera alikuwa miongoni mwa wachezaji waliotambulishwa kwa upande wa Simba lakini baadae akukumbwa na majeruhi ya mara kwa mara kabla ya kuanza kukaa benchi.

"Nimefarijika sana kuona mashabiki wa Simba wakiendelea kuniunga mkono, wameonesha mapenzi kwangu nami nawependa pia, nawatakia kila la kheri katika msimu mpya wa ligi," alisema Kiongera.

Kiongera alicheza kwa dakika 55 pekee katika mchezo huo maalumu wa maadhimisho ya miaka 80 ya klabu ya Simba ambapo Leopards walizidiwa kila Idara.

Aidha mshambuliaji huyo raia wa Kenya alisema kikosi cha Simba cha msimu huu kina mabadiliko makubwa kiuchezaji huku kukiwa na idadi kubwa ya wachezaji vijana.

"Wana timu nzuri, ushauri wangu waendelee kuwaamini wachezaji wao na kuwapa wanachostahili inawezekana wakawa na msimu mzuri katika ligi," alimalizia Kiongera.

Post a Comment

 
Top