BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Moro

TIMU ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni KMC ilisafiri leo kuifuata Simba mkoani Morogoro kwa ajili ya mchezo wa kirafiki ambao umemalizika kwa Wekundu hao kulala kwa bao 1-0.

Bao pekee katika mchezo huo liliwekwa wavuni na Rashidi Roshwa aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Emanuel Memba 'Gatuso' katika dakika ya 10 ambalo lililala hadi mtanange huo unamalizika.


Mshambuliaji mpya wa timu hiyo aliyetokea Azam kwa mkopo Ame Ally 'Zungu' alikosa nafasi za wazi katika kipindi cha kwanza ambazo zingeweza kuwafanya wekundu hao kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa zaidi ya magoli mawili.

Kipindi cha pili Simba walirudi kwa kasi lakini tatizo la umaliziaji liliendelea kuwaandama baada ya Ibrahim Ajib,Mohamed Ibrahim na Said Ndemla nao kukosa nafasi za wazi za kufunga.

Meneja wa Wekundu hao Abbas Ally ameiambia BOIPLUS kuwa matokeo ya mchezo huo hayawaumizi kichwa kwakua ni maandalizi huku kikosi chao kikiendelea kuimarika siku hadi siku.


Kikosi hicho kinatarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam kesho au keshokutwa kwa ajili ya mchezo dhidi ya FC Leorpads ya Kenya katika maadhimisho ya siku ya Simba yatakayofanyika Agosti 8.

Aidha Abasi alisema kuwa wachezaji waliopo katika kikosi hicho watachujwa na Kocha Joseph Omog na kufikia 25 ambao ndiyo atawatumia katika msimu mpya wa ligi utakaoanza Agosti 20.

Post a Comment

 
Top