BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi,Dar
Vicent Angban

KUTOKANA na kufanana kwa viwango vya makipa wa timu ya Simba, kocha wa makipa Adam Meja ameweka wazi kuwa timu hiyo haitokuwa na kipa namba moja badala yake watakuwa wakicheza kwa zamu.

Msimu huu Simba ina makipa watatu  ambao ni Vicent Agban,Manyika Junior waliokuwepo mwaka jana  na Denis Richard aliyekuwa akicheza kwa mkopo katika klabu ya Geita Gold Mining iliyokuwa ikishiriki ligi daraja la kwanza.

Meja ameiambia BOIPLUS kuwa katika vitu ambavyo havimuumizi kichwa ni kufanya uchaguzi wa kipa gani aanze katika mechi licha ya Agban kupewa nafasi kubwa kutokana na uzoefu wake katika mpira.

"Makipa wote wako sawa, viwango vyao viko juu na yeyote anaweza kuanza katika mchezo wowote inategemea na jinsi walivyoamka kwa siku hiyo," alisema Meja.

Manyika Jr

Meja amewachambua makipa hao kwa kusema kuwa kila mmoja ana sifa yake ambapo Agban anatekeleza majukumu yake tu bila kucheza na majukwaa huku Manyika akionekana kuwa bado hajapata uzoefu hivyo kumpelekea kufanya makosa madogo madogo lakini akakiri anaendelea kuwa kipa mzuri.

"Uzuri wa Agban hachezi na jukwaa yeye akiwa langoni anatekeleza majukumu yake tu, Manyika ni mzuri sana na anajituma lakini uzoefu unamkwamisha ila namtabiria atafika mbali," alisema Meja.

Aidha Meja hakusita kumwagia sifa kipa chipukizi Denis kutokana na kujitambua kwake huku akipata nafasi ya kucheza michezo mingi ya ligi daraja kwanza na akatanabaisha kuwa atakuwa msaada mkubwa kwa Taifa katika siku za usoni.

"Bado ni kijana mdogo anajitambua, anajua anachotakiwa kufanya uwanjani pia ana nidhamu kwahiyo kama hatabadilika nae atafika mbali," alisema Meja.

Post a Comment

 
Top