BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu,Dar
KIKOSI cha watoto wa Jangwani mabingwa wa Tanzania Bara na kombe la Shirikisho Yanga kipo kamili 'gado'  kuelekea mchezo wao wa kombe la Shirikisho barani Afrika hatua ya nane bora dhidi  Mo Bejaia ya Algeria. Mtanange huo utapigwa Agosti 13 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kocha msaidizi wa timu hiyo Juma Mwambusi aliitonya BOIPLUS kuwa timu ipo vizuri na inaendelea na mazoezi yake katika viwanja vya Gymkhana huku wachezaji wote wakiwa na ari na kuahidi ushindi katika mtanange huo.

"Wachezaji wapo katika hali nzuri sana kuelekea mchezo huo ambao tunatakiwa kushinda kwa namna yoyote ile  ili kuongeza matumaini ya kufuzu katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Hatujawahi kushinda katika uwanja wetu wa nyumbani zaidi ya kuambulia sare na kufungwa mchezo mmoja, ila tumejipanga kuwafunga hawa Bejaia ili tujiweke katika nafasi nzuri," alisema  Mwambusi.

Katika mtanange huo Yanga itamkosa Nyota wake muhimu Donald Ngoma ambae anatumikia adhabu ya kukosa mchezo mmoja kufuatia kupata kadi za njano katika michezo mitatu tofauti
, washambuliaji Obrey Chirwa na Amissi Tambwe wanatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji.

Kwa upande  wake straika ambaye amekuwa hafanyi vizuri sana kwenye michezo ya kimataifa, Tabwe alisema nafasi bado wanayo ya kusonga mbele na wamedhamiria  kutumia kila nafasi itakayopatikana ili kuibuka na ushindi katika mchezo huo.

"Bejaia ni wazuri ila sisi tumejindaa vizuri zaidi na tuna matumaini ya kushinda kutokana na maandalizi tuliyoyafanya, nawaomba mashabiki wetu waje kwa wingi kwa ajili kutupa nguvu," alisema Tabwe.

Yanga inatarajiwa kumaliza mechi zake za Kundi A za Kombe la Shirikisho kati ya Agosti 23 na 24, mwaka huu huku ikiwa inashika mkia katika kundi lake kwa kuambulia alama moja pekee.

Post a Comment

 
Top