BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Dar
VIONGOZI wa matawi ya klabu ya Yanga wamelaani vikali kauli ya Katibu wa baraza la wazee Mzee Ibrahim Akilimali kumkashifu Mwenyekiti Yusuph Manji kuwa alikurupuka sawa na walivyokurupuka wanachama kwenye kupitisha mchakato wa kumkodisha timu hiyo.

Jana Mwenyekiti wa klabu hiyo alitangaza kutaka kujiuzulu kutokana na maneno yaliyotolewa na Mzee Akilimali ambaye aliukosoa mkutano mkuu uliopitisha mabadiliko yatakayomuwezesha Manji kuikodisha Yanga kwa miaka 10.

Wakizungumza katika makao makuu ya klabu hiyo kwenye kikao cha dharura viongozi hao wameutaka uongozi wa Yanga kumchukulia hatua za kinidhamu Mzee huyo kwakua tabia hiyo ya kuongea na vyombo cha habari pasi na utaratibu imekuwa ikijirudia mara kwa mara.

Aidha viongozi hao walienda mbali zaidi na kusema Katibu huyo anatumiwa na baadhi ya watu ili kuihujumu Yanga ifanye vibaya kitu ambacho ni usaliti mkubwa na hakipaswi kufumbiwa macho.

"Mzee Akilimali ni msaliti mkubwa na hatufai ndani ya klabu yetu na ninauomba uongozi umfute uanachama mara moja ili tubaki salama," alisema Katibu wa tawi la Keko Ukombozi.

Aidha Asubuhi ya leo Mzee Akilimali aliwaomba radhi wanachama wa klabu hiyo baada ya kusema jana kuwa Yanga ilikurupuka kukubali timu yao kukodishwa na Manji kwa miaka kumi.

Post a Comment

 
Top