BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar

MASHABIKI wa Simba juzi mioyo yao ilisuuzika walipomuona straika wao Laudit Mavugo ambaye ujio wake wameusubiri tangu mwaka jana na akawavuruga alipowaambia kufunga kwake ni jambo la kawaida sana pale anapopata nafasi.

Mavugo alifunga bao moja kati ya manne yaliyofungwa na Simba dhidi ya AFC Leopards ya Kenya huku pia akishiriki katika upatikanaji wa mabao mengine mawili. Mechi hiyo maalumu ya maadhimisho ya miaka 80 ya Simba ilichezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salam.

Akizungumza na BOIPLUS, Mavungo ambaye ni raia wa Burundi alisema kuwa huwa hapangi idadi ya kufunga mabao ila ana uwezo wa kufunga zaidi.


"Mechi ilikuwa nzuri na Simba ina mashabiki wengi, nikiingia uwanjani nakuwa na wazo la kufunga ila huwa sijui nitafunga mabao mangapi, mashabiki wasubiri mambo mazuri.

"Wakati nashangilia nilikuwa natoa ishara ya kwamba muda umefika wa wao kufurahi hata mimi nilikuwa nasubiri muda ufike wa kutua Simba ambao ni huu," alisema Mavugo.

Simba imemsajili Mavugo akitokea Vital'O ambako amekuwa mfungaji bora wa ligi ya Burundi akifunga mabao 30 na ameonyesha kuwa na hamu ya kutwaa kiatu cha Dhahabu ambacho msimu uliopita kimebebwa na Mrundi mwenzake Amissi Tambwe.

Post a Comment

 
Top