BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu,
TIMU ya Mbeya City imejipanga kuondoka na alama zote tatu kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mbao FC utakaopigwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba mwishoni wiki hii.

Timu hiyo inatarajia kuondoka mkoani Shinyanga siku ya Ijumaa kuelekea Mwanza tayari kwa mtanange huo dhidi ya wageni hao wa ligi ambao wanaonekana wanaweza wakaleta changamoto msimu huu.

Wagonga Nyundo hao toka jijini Mbeya wanafanya mazoezi kwenye uwanja wa Kambarage kujiweka sawa kabla ya kushuka dimbani Jumamosi ijayo.

Ofisa Habari wa klabu hiyo Dismas Ten alisema kuwa kocha Kinnah Phiri amechagua kuweka kambi ya muda mkoani Shinyanga kabla ya keshokutwa Ijumaa kuelekea Mwanza kutokana na utulivu wa mkoa huo utakaowapa nafasi wachezaji wake kujifua vyema kabla ya mchezo.

“Tumekuwa hapa Shinyanga toka siku ya jumatatu, kwa ajili ya mazoezi na matayarisho. Mwalimu alichagua kufanya mazoezi Kambarage kwa lengo moja tu la kupata utulivu na kuandaa kikosi vizuri ili kuhakikisha tuanshinda na kupata pointi tatu," alisema Ten.

 Aidha Ten aliweka wazi kuwa kiungo Geoffrey Mlawa na mshambuliaji Omary Ramadhani waliopata majeraha kwenye mchezo uliopita dhidi ya Toto Africans wamerejea kwenye hali nzuri na wanaweza kuwa sehemu ya mchezo huo wa jumamosi endapo kocha Phiri atapenda kuwatumia.

"Kwa mujibu wa jopo la madaktari wa timu yetu wamethibitisha wachezaji hao wapo vizuri kikubwa itategemea kocha atapanga vipi kikosi ila kwa sasa nyota hao hawana tatizo," alimalizia Ten.

Post a Comment

 
Top