BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF), limemteua Noiret Jim Bacari wa Comoro kuwa mwamuzi wa kati katika mchezo wa marudiano utakaozikutanisha timu za taifa za vijana za Serengeti Boys ya Tanzania na Amajimbos ya Afrika Kusini, utakaofanyika Agosti 21 Kwenye Uwanja wa Chamazi ulioko Mbagala nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa ya CAF iliyofika Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) mapema wiki hii, waamuzi wasaidizi pia wanatoka Comoro ambao ni washika vibendera Mmadi Faissoil na Said Omar Chebli wakati mezani atakuwa Ali Mohamed Adelaid huku Kamishna wa mchezo huo atatoka Somalia ambaye anaitwa Amir Abdi Hassan.

Jumamosi iliyopita, ikicheza mbele ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kadhalika Naibu Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Rosemary Chambe Jairo, Serengeti Boys ilitoka sare ya 1-1 na Afrika Kusini.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Dobsonville ulioko Soweto, mabao yote yalipatikana kipindi cha pili yakiwa ni ya penalti kwa kila upande.

Serengeti inahitaji ushindi wa aina yoyote kujihakikishia kusonga mbele katika michuano hiyo mikubwa barani Afrika kwa vijana.

Post a Comment

 
Top