BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi,Dar
SIKU moja baada ya kuvuliwa uanachama wa klabu ya Yanga aliyekuwa Mjumbe wa kamati ya Utendaji Salum Mkemi amesema bado ataendelea kuwa mwanachama wa mabingwa hao kwakua mkutano uliofanyika jana ni batili kwa mujibu wa katiba.

Wanachama wa Yanga wakiongozwa na Mwenyekiti wao Yusuph Manji waliwavua uanachama wajumbe wa kamati ya Utendaji Mkemi, Ayub Nyenzi na Hashimu Abdallah kwenye mkutano mkuu wa dharura uliofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee kutokana na kuonekana ni wasaliti wa klabu hiyo.

Mkemi ameambia BOIPLUS kuwa mkutano wa jana ulikuwa batili kwakua ulikiuka katiba ya Yanga ambayo inaeleza endapo Mwenyekiti akitaka kuitisha mkutano wa dharura lazima akae na wajumbe wa kamati ya utendaji siku 30 kabla huku ajenda zikitakiwa kuwekwa wazi siku 15 kabla ya mkutano lakini walishindwa kufanya hivyo.

"Siwezi kufukuzwa uanachama katika mkutano batili uliokiuka katiba ya Yanga. Mimi ni mwanachama halali na hawawezi kunifukuza," alisema Mkemi.

Aidha Mkemi alisema kuwa anajimini na hawezi kupoteza haki yake ndani ya Yanga huku akisema kuwa atatoa tamko ndani ya siku chache zijazo juu ya mustakabali wake kuhusiana na suala hilo.

Alhamisi iliyopita Mkemi alisikika katika kituo kimoja cha radio akiupinga wazi wazi mkutano huo mkuu wa dharura uliofanyika jana kuwa ni batili na umekiuka katiba ya klabu hiyo na kusema hawezi kuhudhuria asilani.

Post a Comment

 
Top