BOIPLUS SPORTS BLOG

LONDON, Uingereza
PAZIA la ligi kuu ya Uingereza limefunguliwa rasmi kwa mchezo wa ngao ya jamii ambapo Manchester United imeibuka na ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya mabingwa watetezi Leicester City katika uwanja wa Wembley.

United walipata goli la kwanza dakika 32 kupitia kwa Jesse Lingard baada ya kuwapita mabeki wa Leicester kutoka katikati ya uwanja kabla ya kumchambua mlinda mlango Gasper Schmichael.

Mabingwa hao walirudi kwa kasi kipindi cha pili ambapo dakika 52 Jamie Vardy aliipatia Leicester goli la kusawazisha baada ya Maroune Fellain kurudisha mpira mfupi kabla ya mshambuliaji huyo kuunasa na kumfunga kirahisi golikipa David De Gea.

Zlatan Ibrahimovic alifunga goli la ushindi dakika ya 83 kwa kichwa akimalizia mpira wa krosi uliopigwa na Antonio Valencia upande wa kulia ambapo mshambuliaji huyo aliwazidi ujanja mabeki wa Leicester.

Hilo ni taji la kwanza kwa kocha Jose Mourinho ambaye  anakinoa kikosi hicho baada ya kuchukua kibarua kilichoachwa na Mholanzi Louis van Gaal aliyetimuliwa mwishoni mwa msimu uliopita.

Post a Comment

 
Top