BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
KLABU ya Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro imelitaka Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF kukubali ombi la timu ya Azam kucheza mechi zake za nyumbani dhidi ya Simba na Yanga kwenye uwanja wao wa Azam Complex.

Jana klabu ya Azam kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake Nassor Idrisa walipeleka TFF barua ya kuomba mechi zao za nyumbani dhidi ya Miamba hiyo ya soka nchini zichezwe kwenye uwanja wa Azam Complex ili nao wafaidike kwakua dhamira ya kujengwa kwa dimba hilo  ni kuwafanya Wana lambalamba wafanye vizuri kwenye michezo yao.

Mtibwa kupitia kwa Ofisa Habari wake Thobias Kifaru wameitaka TFF kukubali ombi hilo ili kuwaamsha Simba na Yanga kujenga viwanja vyao nakuacha kutumia uwanja wa Taifa ili haki itumike na kupunguza uwezekano wa upangaji wa matokeo.

"Uwanja wa Azam Complex ni miongoni mwa viwanja bora Afrika Mashariki na kati kama umeruhusiwa kuchezwa kwa mechi zinazotambuliwa na FIFA kwanini Simba na Yanga wasicheze pale," alihoji Kifaru.

Aidha Kifaru alisema kwa upande wa mechi zao za nyumbani dhidi ya miamba hiyo kuchezwa kwenye uwanja Jamhuri na sio Manungu Complex ni kutokana na wao kuwaandikia barua TFF mwaka 1998 kwa sababu dimba hilo ni dogo na haliwezi kubeba mashabiki wa klabu hizo kongwe nchini.

"Sisi tuliandika barua mwaka 1998 kuomba mechi zetu zichezwe kwenye uwanja wa Jamhuri kwakua Simba na Yanga zina mashabiki wengi nchini," alisema Kifaru.

Timu za Azam, Mtibwa, Ruvu shooting, Mwadui na JKT Ruvu zinatakiwa kuhama uwanja wa nyumbani zinapocheza dhidi ya Simba na Yanga kwakua miamba hiyo ina mashabiki wengi ambao hawawezi kutosha kwenye viwanja hivyo.

Post a Comment

 
Top