BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
Mzee Akilimali akiwa na wanachama wenzake wa Yanga wakielekea jijini Kigali Yanga ilipoivaa APR kwenye klabu Bingwa Afrika

WANACHAMA wa  Yanga wameambiwa wamekurupuka kukubali kirahisi kumkodisha Mwenyekiti wao Yusuph Manji klabu hiyo kwakua suala hilo halikufanyika kisheria.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa baraza la wazee wa klabu hiyo Mzee Ibrahim Akilimali na kukiri kuwa yeye anaupinga mchakato huo kwavile inaonekana mwisho wake hautakuwa mzuri kwa upande wa Yanga.

Mzee Akilimani ameyazungumza hayo katika kituo cha radio cha EFM kwenye kipindi cha Sports Headquarters asubuhi ya leo ambapo alisema kuwa mwaka 2006 Mwenyekiti huyo ndiye aliyetaka timu hiyo iwe kampuni huku Yanga ikitakiwa kuwa na hisa 51% na wawekezaji 49%.

"Yeye mwenyewe Manji mwaka 2006 alituambia endapo tutabadili mfumo na kuwa kampuni basi klabu itatakiwa kumiliki hisa 51% sasa leo mbona anataka kutugeuka na kuchukua 75%?," alihoji Mzee Akilimali.

Aidha Mzee Akilimali alisema mchakato huo haukupaswa kwenda haraka kiasi hicho kwakua wanachama hawakuwa na uelewa mkubwa kuhusu suala hilo na ndiyo maana walitoa maamuzi ambayo hawakuyajua hatima yake itakuwaje siku za usoni.

Katibu huyo alisema pia endapo azma ya Manji itatimia ya kuikodisha klabu hiyo hajui hatma ya viongozi wengine waliochaguliwa na wanachama kwenye uchaguzi mkuu  uliopita watakuwa na majukumu gani.

Post a Comment

 
Top