BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
WAZIRI wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Nape Nnauye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa kongamano la Jukwaa la kandanda  litakalofanyika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam siku ya Jumamosi na Jumapili.

Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ambaye pia ni mkufunzi wa Shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA Henry Tandau amewaambia waandishi wa Habari kuwa dhamira ya kongamano hilo ni kujadili masuala ya soka ili kulikwamua toka hapa lilipo na kulisogeza mbele zaidi.

Tandau alisema pia kongamano hilo pia litatumika kurasimisha Jukwaa hilo na kutambulika kisheria kwa mujibu wa katiba ya nchi ambapo wadau mbalimbali wa soka wataruhusiwa kutoa maoni yao kuhusu kitu gani kifanyike ili kuinua mpira wa miguu nchini.

"Tunatarajia mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Habari kwakua naye ni miongoni mwa wanachama wa Jukwaa hili. Dhamira yetu ni kuliinua soka letu kutoka hapa lilipo kusonga mbele zaidi" alisema Tandau.

Tandau pia alizitaja mada zitakazo jadiliwa kwenye kongamano hilo kuwa ni Uongozi na Utawala bora pamoja na leseni za klabu ili kusaidia kuwafahamisha wadau kwa undani kuhusu hilo.

Miongoni mwa washiriki wa kongamano hilo ni pamoja na Bodi ya ligi(TPLB),Wajumbe toka TFF,Wadhamini wa Jukwaa hilo, Viongozi wa klabu, Baraza la michezo( BMT) bila kusahau Waandishi wa Habari.

Post a Comment

 
Top