BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
HATI za kimataifa za uhamisho (ITC) za wachezaji wawili wa Simba raia wa DR Congo zinatarajiwa kuwasili nchini muda wowote kutoka sasa ili kuanza kutumika kwenye michezo ya ligi kuu.

Wachezaji hao ni beki wa kulia Janvier Bukungu pamoja na kiungo Musa Ndusha ambao hawajecheza michezo yote miwili ambayo Simba imeshuka dimbani tangu kuanza kwa ligi Agosti 20.

Katika michezo ya maandalizi pamoja na ule wa Simba Day dhidi ya AFC Leopards ya Kenya nyota hao walishuka dimbani na kuonesha wanaweza kufanya vizuri endapo watapewa muda na kuaminiwa.

Ofisa Habari wa klabu hiyo Haji Manara amewaambia waandishi kuwa wamewasiliana na chama cha mpira wa miguu cha DR Congo ambao wamewaambia watawatumia siku chache zijazo.

"Tunategemea kupokea ITC za wachezaji wetu raia wa Congo siku chache zijazo kwakua tumewasiliana na wenzetu wa kule wamesema watatutumia muda si mrefu," alisema Manara.

Wachezaji hao wamejumuishwa kwenye kikosi cha Simba kitakachosafiri keshokutwa kuelekea mkoani Dodoma kwa ajili ya mchezo maalum dhidi ya Polisi Dodoma utakaopigwa Septemba 3.

Post a Comment

 
Top