BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally
STRAIKA wa zamani wa Yanga, Paul Nonga ameonyesha makali yake baada ya kuifungia timu yake mpya ya Mwadui mabao yote mawili katika ushindi wa mabao 2-0 kwenye mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa jioni ya leo kwenye Uwanja wa Mwadui Complex dhidi ya Black Eagle ya Burundi.

Nonga ambaye anaichezea Mwadui kwa mkopo alionyesha kiwango cha juu ingawa alikosa bao la wazi kabisa kipindi cha pili baada ya mpira kudunda akiwa yeye na kipa na mpira kutoa nje.

Mechi hiyo ni mwendelezo wa maandalizi ya Ligi Kuu Bara inayotarajia kuanza wiki ijayo ambapo kikosi hicho kinaangaliwa endapo kuna mapungufu katika safu zao ili kufanya marekebisho ya kiufundi mapema.

Nonga alifunga bao la kwanza katika kipindi cha kwanza wakati la pili akilifunga kipindi cha pili kwa kuunganisha krosi safi ya Hassan Kabunda. 

Nonga alionekana mwenye bahati na mechi hiyo ingawa alipoteza baadhi ya nafasi alizozipata ambazo angeweza kuzitumia kuipatia mabao zaidi kutokana na Warundi hao wakishambuliwa mara kwa mara.

Mwadui ni miongoni mwa timu ambazo zimefanya mabadiliko makubwa kwenye usajili ambapo wamewaongeza nyota kama Nasoro Masoud 'Chollo' aliyekuwa nahodha wa mechi hiyo, Abdallah Seseme, Salum Kanoni  pamoja na Joseph Kimwaga.

Post a Comment

 
Top