BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, Shinyanga
BEKI wa zamani wa Simba, Joseph Owino amefurahishwa na kitendo cha yeye kurudi kucheza Ligi Kuu Bara huku akitamba kuwadhihirishia uwezo wale waliomdharau akiwa Simba.

Owino ambaye amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuichezea Stand United akitokea URA ya Uganda, anajiamini kuwa yeye bado ni mchezaji bora kati ya wachezaji wa kulipwa waliopo nchini. 

Akizungumza na BOIPLUS, Owino alisema kuwa Stand United ni timu nzuri na yenye malengo ukiachana na mambo ya kiuongozi yanayoendelea sasa bali yeye anachojali ni namna gani timu hiyo itafanya vyema msimu ujao. 

"Wachezaji wengi huwa wanaumia wanapokalishwa benchi, nilikaa benchi nikiwa Simba lakini bado sikutaka kumchukia mtu kwani nilijua kiwango changu kikoje, najiamini kwa kila ninachokifanya na huwa nafanya mambo yangu kwa nidhamu kubwa.

"Maisha ya Simba siku za mwisho yalikuwa ni ya kukatisha tamaa ila sikutaka kukata tamaa kwani ningepoteza kiwango changu, nipo Stand sasa nataka niwaonyeshe mashabiki kuwa bado ninaweza kucheza," alisema Owino.

Kocha wa Stand United, Patric Liewig naye ametamba juu ya usajili wake kwamba anachokitegemea msimu ujao ni kumaliza ligi akiwa kwenye tano bora huku akimsifu Owino kwa uwezo wake. 

"Tuna malengo yetu kama nilivyojiwekea msimu uliopita kwamba nitamaliza nikiwa kwenye nane bora na sasa nataka tano bora, naamini nitaweza," alisema Liewig

Post a Comment

 
Top