BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally
KOCHA mkuu wa Mbeya City, Kinnah Phiri ameweka wazi kwamba kumkosa straika wake mpya Mohamed Mkopi katika mechi yao ya leo dhidi ya Kagera Sugar kumepunguza makali ya safu ya ushambuliaji ambako kumepelekea kukosa mabao mengi.

Mkopi amefungiwa kucheza soka kwa mwaka mmoja na Shirikisho la Soka nchini (TFF) baada ya kubainika kuwa ana mikataba miwili tofauti ya timu mbili, wa kwanza na timu yake ya zamani ya Prisons na huu mpya aliosaini na City.

Phiri alisema kuwa timu yake imeshindwa kutamba kwa wenyeji wao Kagera na kutoka sare tasa katika mechi yao ya kwanza ya ligi kuu Bara iliyochezwa Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.

"Tumepata nafasi nyingi lakini wachezaji wangu wameshindwa kuzitumia, hata hivyo naamini pia kikosi changu kingekuwa kimekamilika bila kumkosa Mkopi huenda tungepata mabao.

"Ni suala la kufanyia kazi tatizo hilo kabla ya mechi yetu ijayo dhidi ya Toto African pamoja na Mbao FC, pia mara nyingi mechi ya kwanza ya ligi huwa ni ngumu kupata matokeo mazuri," alisema Phiri.

Mbeya City imevuna pointi moja na itaendelea kupiga kambi mjini Shinyanga ambapo itakuwa ikifanya mazoezi yake Uwanja huo wa Kambarage na wataifuata Toto jijini Mwanza, Ijumaa.

Post a Comment

 
Top