BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu,Dar
BAADA ya kusuasua kwa safari ya winga wa timu ya Azam FC Farid Mussa kwenda kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Tenerife inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini Hispania, dili hilo sasa liko mbioni kukamilika.

Miezi mitatu iliyopita winga huyo  alienda kufanya majaribio kwenye timu hiyo na kufuzu lakini safari yake ya kwenda nchini Hispania imekuwa na sintofahamu nyingi lakini hivi sasa inaelekea kukamilika.

Farid ameiambia  BOIPLUS kuwa   safari yake ya kwenda Hispania ipo pale pale na kila kitu viongozi wa Azam wanasimamia na wamefikia pazuri na anaamini muda si mrefu atasafiri.

“Kinachokwamisha safari yangu ni visa ilichelewa ila muda si mrefu kila kitu kitakaa sawa,  Kwasasa bado nipo chini ya Azam na wananilipa mshahara kama kawaida,” alisema Farid.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo Saad Kawemba alisema kila kitu kinakwenda sawa kwakua tayari  wameshamsainisha mkataba winga huyo ila kinachocholewesha ni visa ambayo ikipatikana muda wowote nyota huyo atasafiri. 

“Mikataba yote ya yeye kuhama kutoka Azam kwenda Tenerife tumeshasaini  kwa sasa tunaiandaa  ITC yake kabla ya kutumiwa tiketi na kwenda huko Hispania," alisema Kawemba.

Endapo mpango huo utafanikiwa Farid atakuwa ameongeza idadi ya wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania wanaocheza nje nchi ambao mara nyingi wamekuwa na msaada mkubwa kutokana na uwezo wao.

Post a Comment

 
Top