BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu
TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’, kesho Jumamosi itashuka dimbani kumenyana na wenyeji Afrika Kusini katika Uwanja wa Dobsonville ulioko Soweto, kwenye  mchezo wa awali kuwania nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, zitakazofanyika Madagascar mwakani.

Kocha mkuu wa Serengeti boys Bakari Shime amejinasibu kuwa wataibuka na ushindi katika mchezo huo kutokana na vijana wake kuyafanyia kazi mafundisho yake anayowapa.

 “Tutaifunga Afrika Kusini hapa kwao hilo linawezekana japokuwa hata wao wamejipanga tutajitahidi kutumia nafasi tutakazopata ili mechi ya marudiano iwe nyepesi kwetu” alisema Shime.

Mchezo huo utakaoanza saa 9.00 alasiri kwa saa za Afrika Kusini wakati huku Tanzania itakuwa ni saa 10.00 jioni katika uwanja ambao hutumiwa na timu ya Moroka Swallows ambayo kwa sasa imeshuka daraja hadi la pili.

 Mchezo huo kwa Serengeti Boys  utakuwa ni mtihani wa kwanza kati ya miwili kabla ya kufuzu kuelekea Madagacar. Mchezo wa kwanza unafanyika Afrika Kusini, kabla ya kurudiana Agosti 21 katika Uwanja wa Azam ulioko Chamazi-nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Aidha kocha Shime alishukuru mipango na ahadi ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kugharamia kambi ya siku 10 iliyoyofanyika Madagascar akisema: “Ilikuwa ni kambi bora. Kwa sasa kikosi changu kinahitaji kulipa deni la Watanzania na ahadi ya Rais Malinzi kwa kuibuka na ushindi katika mchezo huo”.

Post a Comment

 
Top