BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Chamazi
TIMU ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 Serengeti Boys wamejiweka kwenye hatua nzuri ya kufuzu fainali za Afrika kwa vijana baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Afrika Kusini 'Amajimbosi' kwenye mchezo wa marudiano uliofanyika katika uwanja wa Azam Complex.

Katika mchezo wa awali timu hizo zilitoka sare ya kufungana goli 1-1 wiki mbili zilizopita nchini Afrika Kusini.

Serengeti walionesha kandanda safi kipindi cha kwanza na kuwaacha Amajimbos wakiwa hawaamini kilichokuwa kikitokea katika mtanange huo lakini baada ya mchezaji wao kutolewa kwa kadi nyekundu walipunguza mashambulizi.

Dakika ya 36 Mohamed Rashidi aliipatia Serengeti goli la ufunguzi baada ya kumalizia krosi safi ya Israel Patrick upande wa kulia wa uwanja.

Mchezaji Ally Hamisi alioneshwa kadi ya pili ya njano dakika ya 45 iliyopelekea kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu mbaya mchezaji wa Amajimbos.

Mshambuliaji Muhsini Makame aliipatia Serengeti goli la pili dakika ya 85 kufutia mpira wa krosi uliopigwa na Mohamed Rashidi.

Serengeti sasa itamenyana na mshindi kati ya Namibia na Congo Brazaville na endapo itashinda katika mchezo huo itafuzu moja kwa moja kwa fainali za Afrika zitayofanyika nchini Madagascar.

Post a Comment

 
Top