BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
SERIKALI ipo tayari kuandaa kikao maalum kitakacho zikutanisha pande mbili zinazokinzana za timu ya Stand United ili kumaliza mgogoro unaoendelea kuitafuna klabu hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Nape Nnauye alipokuwa akizungumza na Waandishi kuhusu mgogoro wa timu hiyo unavyoweza kasababisha kupotea kwa Wapiga debe hao kwenye medani ya Soka nchini.

Waziri Nape amezitaka pande mbili zinazovutana kukaa chini kuzungumza na kulimaliza suala hilo kwakua ndiyo njia pekee ya kutafuta suluhu ambayo itainusuru timu hiyo.

Kwa muda mrefu sasa timu ya Stand imekuwa na mgororo ambao baadhi ya watu wanataka iwe kampuni huku wengine wakitaka iendelee kubaki chini ya wanachama kama ilivyokuwa wakati ikianzishwa.

"Ili kuondoa mgogoro huo pande zote zinatakiwa zikutane zikae chini wamalize tofauti zao  kwa mazungumzo ili kuinusuru timu hiyo," alisema Nape.

Wakati huo huo Waziri Nape alisema kuwa mfumo wa tiketi za Kielectoniki utafungwa kwenye viwanja viwili pekee vya Serikali ambavyo ni Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Uhuru kwakua hivyo ndiyo wana mamlaka navyo.

"Viwanja vingine ni vya Chama na watu binafsi kwahiyo hatuna mamlaka navyo, vya kwetu ni viwili tu ambavyo vitatumia mfumo huo," alisema Nape.

Septemba 4 mfumo huo utakuwa umekamilika na utakabidhiwa kwa Serikali tayari kwa kuanza kutumika.

Post a Comment

 
Top