BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
KIKOSI cha timu ya Simba kitasafiri keshokutwa Alhamisi kuelekea mjini Dodoma baada ya kupata mwaliko maalum kutoka kwa chama cha soka mkoani humo.

Simba itashuka dimbani siku ya Jumamosi Septemba 3 kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Polisi Dodoma inayoshiriki ligi daraja la kwanza ambayo imejidhatiti kurejea ligi kuu msimu ujao.

Mwenyekiti wa chama cha mpira wa miguu mkoani Dodoma (DOREFA) Mulamu Ng'ambi amewaambia waandishi wa Habari kuwa mechi hiyo pia itatumika kama jitihada za kuiunga mkono Serikali ya kuhamishia makao makuu mkoani Dodoma.

"Mechi hiyo itakuwa kwa ajili ya kuziandaa timu zote baada ya mapumziko kupisha mechi za kimataifa lakini pia ni kuunga mkono jitihada za Serikali kuhamia Dodoma," alisema Ng'ambi.

Kwa upande wake Ofisa Habari wa Simba Haji Manara kwa niaba ya uongozi wa klabu hiyo amewashukuru DOREFA kwa mwaliko huo ambao utawasaidia wapenzi wa timu hiyo kukiona kikosi cha Wekundu hao ambao wamekikosa kwa zaidi ya miaka kumi.

"Tunawashukuru DOREFA kwa mwaliko huu, pia tutaumia mchezo kuwaonesha kikosi chetu kwa wakazi wa mkoa wa Dodoma ambao ni wengi sana" alisema Manara.

Post a Comment

 
Top